Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utu na fursa kwa wote vinategemea upatikanaji wa makazi bora: Ban

Utu na fursa kwa wote vinategemea upatikanaji wa makazi bora: Ban

Leo ikiwa ni siku ya makazi duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema utu na fursa kwa wote vinategemea upatikanaji wa makazi bora kwa gharama nafuu. Rosemary Musumba na taarifa kamili.

(Taarifa ya Rosemary)

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hiyo, Ban amesema kwa kutambua umuhimu wa makazi bora kwa maendeleo , mkutano wa tatu wa makazi ujulikanao kama Habitat III utafanyika Quito Equado baadaye mwezi huu na kujikita katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030.

Kwa mujibu wa Ban kufikia malengo hayo 17 ya maendeleo endelevu kutategemea kwa kiasi kikubwa endapo itawezekana kuifanya miji na makazi kujumuisha wote, kukabiliana na changamoto na kuwa endelevu.

Amesema hilo ndio lengo la ajenda mpya ya miji, ambayo serikali na wadau wa maendeleo watatarajiwa kuipitisha kwenye mkutano wa Quito.

Zaidi ya nusu ya watu wote duniani wanaishi katika maeneo ya mijini, huku karibu robo yao wanakaa katika mitaa ya mabanda na makazi yasiyo rasmi.