Serikali ziwe na mipango ya kitaifa ya mtandao wa intaneti

Serikali ziwe na mipango ya kitaifa ya mtandao wa intaneti

Mkutano kuhusu upatikanaji wa mtandao wa intaneti duniani unafanyika hii leo jijini New York, Marekani, kuangazia ni jinsi gani serikali zinaweza kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo adhimu kama njia mojawapo ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa  kuhusu SDGs, David Nabarro amewasilisha ujumbe wa katibu mkuu wakati huu ambapo ripoti kuhusu upatikanaji wa mtandao wa intaneti ilibaini kuwa asilimia 55 ya wakazi wa dunia hawajawahi kutumia huduma hiyo.

Masuala makuu katika mjadala wa leo ni jinsi gani ya kutumia mtandao wa intaneti hasa ule unaopatikana majumbani, shuleni na hospitali ili kuchochea huduma hizo pamoja na uwekezaji na hatimaye kuondoa pengo kati ya walio na huduma hiyo na wasio nayo.

Mwandishi wa ripoti hiyo Phillipa Biggs kutoka tume ya Umoja wa Mataifa ya mtandao wa intaneti, akihojiwa na Idhaa hii amesema..

“Jambo muhimu ni kwa serikali kuwa mtazamo kwenye  mpango wa kitaifa wa huduma ya intaneti, na mpango huo upatiwe kipaumbele na ushirikishe wizara na watunga sera mbali mbali ili uweze kunyumbulika katika utekelezaji na ujumuishe sekta zote.”