Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saa 48 tunazotaka si mbinu ya kujadili bali kupeleka misaada- O’Brien

Saa 48 tunazotaka si mbinu ya kujadili bali kupeleka misaada- O’Brien

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu ndani ya Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien amelieleza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa saa 48 za sitisho la mapigano nchini Syria si mbinu ya kuwezesha mashauriano bali lengo kuu ni kuwezesha misaada muhimu iwafikie wahitaji.

Akihutubia baraza hilo leo O’Brien amesema kwa mantiki hiyo anaomba nchi zenye ushawishi mkubwa kwa Syria zifikie makubaliano haraka ya kusitisha mapigano kwenye mji wa Aleppo na maeneo mengine nchini humo.

Amesema magari yenye shehena za misaada yako tayari kuanza safari pindi kibali kitakapotolewa na huku akieleza kuchukizwa kwake kuwa uharibifu nchini Syria unaendelea kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

"Kinachofanyia Aleppo leo na kwingineko Syria kwa zaidi ya miaka mitano ni uharibifu wa kila maadili yetu sisi binadamu, kwa kuwa binadamu wenzetu raia wa Syria wamekumbwa kwenye mzozo usiomalizika. Na huku ni kushindwa kwa siasa, kushindwa kwetu sote, unafahamu hili kama baraza la usalama. Kwa hiyo tafadhali huu ni wakati, sasa hivi tuweke tofauti zetu kando, tuwe kitu kimoja, na kwa pamoja tunaweza aibu hii ya kibinadamu dhidi yetu kwa sasa na kwa wakati wote.”