Sudan Kusini yakubali kikosi kutoka ukanda wa IGAD, Ban apongeza

7 Agosti 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha taarifa ya pamoja iliyotolewa na wakuu wa nchi wa mamlaka ya IGAD na nchi shirika kuhusu mzozo wa Sudan Kusini.

Ban katika taarifa kupitia msemaji wake amepongeza viongozi hao wa IGAD kwa hatua yao ya maamuzi huku akikaribisha pia hatua ya serikali ya Sudan Kusini ya kukubali kupelekwa kikosi cha ulinzi kutoka ukanda huo.

Sambamba na hilo Katibu Mkuu ametoa wito kwa viongozi wote wa Sudan Kusini kuweka kando tofauti zao na kuonyesha utayari wao wa kutekeleza makubaliano kuhusu suluhu la mzozo nchini mwao, makubaliano ambayo amesema ndiyo njia pekee ya kumaliza mzozo.

Amesema anasalia na hofu kubwa kuhusu mapigano yanayoendelea nchini Sudan Kusini na zaidi ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana.

Ametaka pande zote kuwajibika kulinda raia huku akisema anaendelea na azma yake ya kushirikiana na wasudani kusini wote, IGAD, muungano wa Afrika na wadau wa kimataifa kutekeleza maazimio ya mkutano wa viongozi wa IGAD.

Nchi wanachama wa IGAD ni Eritrea, Kenya, Somalia, South Sudan, Sudan na Uganda.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter