Skip to main content

UNHCR yaomba dola milioni 115 zaidi kusaidia wanaorejea kwa hiari kutoka Dadaab

UNHCR yaomba dola milioni 115 zaidi kusaidia wanaorejea kwa hiari kutoka Dadaab

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR), limetoa ombi la dola milioni 115.4 zaidi ili kufadhili usaidizi kwa Wasomali wanaorejea nyumbani kwa hiari kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab, nchini Kenya.

Ombi hilo linafuatia tangazo la serikali ya Kenya mnamo tarehe Sita Mei kuwa imeamua kuifunga kambi ya Dadaab, ambapo UNHCR iliwasilisha mpango wa hatua za kuchukuliwa ili kupunguza idadi ya watu kwenye kambi ya Dadaab kutoka zaidi ya 343,000 hadi 150,000 ifikapo mwishoni mwa 2016.

Ufadhili pia unahitajika kusaidia kuwahamishia wakimbizi wengine 31,000 kwenye kambi ya Kakuma, kutoka Dadaab, pamoja na miradi mingine ya miundombinu Kenya na Somalia.

Awali, UNHCR ilikuwa imeomba dola milioni 369.4 kwa ajili ya athari za hali nchini Somalia, lakini sasa majukumu mapya yameilazimu kufanyia marekebisho kiasi cha fedha zinazohitajika kwa jitihada zake katika nchi zilizoathiriwa hadi dola milioni 484.8. Nchi hizo ni Djibouti, Ethiopia, Kenya na Somalia.