Mtaalam wa UM ataka hatua zaidi kuhusu albino Afrika
Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Ikponwosa Ero, amesema wakati umewadia wa kupunguza maneno na kuchukua hatua kuhusu hatma ya watu hao wanaokabiliwa na unyanyapaa na ukatili barani Afrika.
Bi Ero amesema hayo kabla ya kongamano la kwanza kabisa la kuchukua hatua kuhusu hatma ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ambalo litafayika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 17 hadi 19.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Bi Ero, linalenga kutunga mikakati ya kupambana na mashambulizi na ubaguzi unaowakabili watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi kadhaa kwenye ukanda huo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Watu wenye ulemavu wa ngozi barani Afrika wanakambiliwa na ukiukwaji mbaya zaidi wa haki za binadamu, wakishambuliwa kimwili kwa imani potofu kwamba viungo vya miili yao vinaweza kutumiwa katika hirisi na vitendo vingine vya kishirikina.