Skip to main content

Nchi zinazoibuka kiuchumi zawekeza zaidi kwenye nishati endelevu- Ripoti

Nchi zinazoibuka kiuchumi zawekeza zaidi kwenye nishati endelevu- Ripoti

Ripoti mpya iliyotolewa leo imesema uwekezaji katika nishati endelevu duniani ulifikia dola bilioni 286 mwaka jana na vyanzo husika vya nishati viliwekwa katika maeneo husika kwa kasi kubwa zaidi kuwahi kutokea.

Ikiangazia hali ya nishati endelevu ulimwenguni, ripoti kwa mujibu wa mtandao wa ClimateAction inataja nishati husika kuwa ni ile ya jua, upepo na maji na kwamba uwekezaji wake uliongezeka maradufu ikilinganishwa na uwekezaji kwenye mitambo inayotumia makaa ya mawe na gesi.

Nchi zinazoibuka kiuchumi ndizo ziliwekeza zaidi kwenye nishati endelevu kuliko zile zilizoendelea na hii ni mara ya kwanza kabisa na hatua hiyo imetoa fursa za ajira kwa watu zaidi ya Milioni Nane.

Nchi zinazoendelea ambazo zilizoongoza zaidi kuwekeza kwenye nishati endelevu ni Mauritania, Honduras, Uruguay na Jamaica.

Hata hivyo utafiti huo umesema licha ya uwekezaji kwenye nishati endelevu huko Ulaya kupungua kwa asilimia 21 katika kipindi husika, bado nishati salama ndio chanzo cha umeme kikiwa na asilimia 44 ya vyanzo vya umeme kwenye nchi za Muungano wa Ulaya.