Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo dhidi ya Sudan Kusini vyaendelezwa

Vikwazo dhidi ya Sudan Kusini vyaendelezwa

Baraza la Usalama limekutana leo kujadili hali ya usalama Sudan Kusini na limeamua kuendeleza vikwazo dhidi ya baadhi ya watu binafsi nchini humo.

Kwenye azimio lililopitishwa leo, wanachama wa Baraza hilo wamekaribisha kuundwa kwa serikali jumuishi mnamo tarehe 29 Aprili mwaka huu wakisema ni hatua muhimu katika kutatua mzozo nchini humo. Licha ya hayo wamesikitishwa na jinsi viongozi walivyoshindwa kutimiza ahadi zao kuhusu makubaliano ya amani, ikiwemo kushindwa kutekeleza sitisho la mapigano.

Vikwazo vilivyoamuliwa ni vizuizi vya kifedha na usafiri dhidi ya baadhi ya watu wanaoshukiwa kujihusisha na mashambulizi nchini humo na vitendo vingine vikiwemo ukiukaji wa haki za binadamu, mashambulizi dhidi ya walinda amani na mashirika ya kibinadamu, na vitendo vyovyote vinavyolenga kukwamisha mchakato wa kisiasa.

Kwa hiyo mamlaka za kamati ya wataalam yenye jukumu la kufuatilia vikwazo hivyo zimeongezwa kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja.