Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sababu kubwa ya vifo CAR siyo silaha bali utapiamlo: OCHA

Sababu kubwa ya vifo CAR siyo silaha bali utapiamlo: OCHA

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, sababu kubwa ya vifo vya watoto siyo silaha, bali ni utapiamlo, malaria, ugonjwa wa kuhara na numonia. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na mashirika ya kibinadamu.

Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA imeeleza kwamba kiwango cha utapimalo kimeongezeka na hivi sasa mtoto mmoja kati ya sita nchini CAR anakumbwa na utapiamlo wa kupindukia kwenye majimbo 11 kati ya 16 nchini humo.

Mzozo unaoendelea kwa miaka mitatu umehatarisha zaidi hali ambayo tayari ilikuwa mbaya.

Halikadhalika, idadi ya watu wanaokumbwa na njaa imefikia asilimia 50, kutokana na ukosefu wa mvua, na bei kubwa ya bidhaa.

Dola milioni 531 zinahitajika mwaka huu kusaidia watu wapatao milioni 1.9 nchini humo.