Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masahibu yanayokumba wasaka hifadhi yatia hofu UNHCR

Masahibu yanayokumba wasaka hifadhi yatia hofu UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeeleza wasiwasi wake juu ya masahibu yanayoendelea kukumba wahamiaji na wakimbizi wanaosaka kuingia Ulaya likigusia zahma iliyotokea jana kwenye mpaka wa Ugiriki na Macedonia.

Katika taarifa yake, UNHCR imesema matumizi ya mabomu ya kutoa machozi kulikoenda sambamba na ghasia karibu na mji wa Eidomeni yanapaswa kuangaliwa kwa umakini na pande zenye shuku juu ya hatua za Ulaya dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.

UNHCR imesema iko tayari kusaidia mipango ya kusafirisha watu kwa hiari kuelekea maeneo ambayo yametengwa na serikali ya Ugiriki, ikiwemo kuwasajili na kuwapatia huduma muhimu.

Halikadhalika imesema uamuzi wa kuwahamisha wale wenye sifa za kupta hifadhi ya kimataifa ulishapitishwa na kinachotakiwa sasa ni utekelezaji.