Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu ni muhimu, watu ndio kiini cha Ajenda 2030- Ban

Takwimu ni muhimu, watu ndio kiini cha Ajenda 2030- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa takwimu zina umuhimu mkubwa katika kufanikisha ajenda ya mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu (SDGs), huku akiongeza kuwa watu ndio kiini cha Ajenda hiyo.

Ban amesema hayo katika ufunguzi wa kikao cha 49 cha Kamisheni kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo, ambacho amekitaja kuwa chenye umuhimu mkubwa kwani ndicho cha kwanza tangu kupitishwa Ajenda ya Maendeleo Endelevu.

“Masuala ya ajenda yenu ni nguzo ya malengo ya maendeleo endelevu. Matamanio haya ya mabadiliko ni wito kwa nchi zote ziweze kuwatambua walio wanyonge, kuwasaidia, na kufanyia tathmini hatua zinazopigwa.”

Katibu Mkuu amesema watu daima hawawezi kuzingatiwa kama takwimu tu, lakini takwimu ni muhimu katika kufuatilia hatua za maendeleo..

“Watu wasipohesabiwa, hawajumuishwi. Ili kutimiza ahadi ya kutomwacha mtu yeyote nyuma, ni lazima tuhakikishe kila mtu amehasibiwa. Serikali zitahitajika kukusanya takwimu za hesabu ya watu na kuzitumia katika kuelewa mabadiliko ya idadi ya watu. Hilo litawasaidia kubuni mipango ipasayo.”