Ban aomba jamii ya kimataifa isaidie kukarabati kambi ya Nahr El-Bared, Lebanon

Ban aomba jamii ya kimataifa isaidie kukarabati kambi ya Nahr El-Bared, Lebanon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa itoe ufadhili wa dola milioni 200 zilizosalia ili kukamilisha ukarabati wa kambi ya Nahr El-Bared nchini Lebanon, na kuwezesha wakimbizi wa Palestina kurejea makwao kwenye kambi hiyo. Ban amesema hayo leo alipoizuru kambi hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini Lebanon.

Mnamo mwaka 2007, mapigano kati ya Fatah al-Islam na vikosi vya jeshi vya Lebanon yalilazimu jumla ya wakimbizi takriban 26,000 wa Kipalestina na wenyeji wa Lebanon 1,000 kuihama kambi ya Nahr el-Bared, na kuacha nyumba na vitega uchumi vyao.

Baada ya mzozo huo kuisha, serikali ya Lebanon na jamii ya kimataifa ziliahidi kuikarabati kambi hiyo iliyoharibiwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, lilipewa jukumu la kusimamia usaidizi na jitihada za kukarabati kambi hiyo, na likaanza kazi ya ukarabati. Ban amesema kuikarabati kambi hiyo limekuwa jambo la kipaumbele tangu alipochukua wadhfa wa Katibu Mkuu mnamo mwaka 2007.

"Sasa baada ya miaka tisa, naona takriban nusu ya kazi ya ukarabati imefanyika, lakini bado kuna watu wengi sana wanaorejea kurudi majumbani kwao. Tuna upungufu wa takriban asilimia 45 ya ufadhili. Imechukua muda mrefu sana, ni zaidi ya miaka tisa. Tutakuwa na mkutano wa kibinadamu Istanbul mwezi Mei, na hilo litakuwa moja ya vipaumbele ili tuwezeshe kuwasaidia hawa wakimbizi na malengo ya maendeleo endelevu, ambayo yaliridhiwa mwezi Septemba mwaka uliopita."