Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wasichana mara mbili ya ile ya wavulana hawatoanza shule kamwe:UNESCO

Idadi ya wasichana mara mbili ya ile ya wavulana hawatoanza shule kamwe:UNESCO

Takribani wasichana milioni 16 wenye umri wa kati ya miaka 6 na 11 asilani hawatopata fursa ya kusoma wala kuandika kwenye shule za msingi , ikilinganishwa na wavulana milioni 8, iwapo hali ya sasa itaendelea, kwa mujibu wa ripoti kutoka taasisi ya takwimu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sanyansi na Utamaduni( UNESCO )

. Grace Kaneiya na taarifa kamili.

(Taarifa ya Grace)

Katika kuelekea siku ya kimataifa ya wanawake hapo Machi 8 takwimu hizo za UNESCO kuhusu “usawa wa kijinsia katika elimu” zinaonyesha kwamba wasichana bado ni wa kwanza katika kunyimwa haki ya elimu licha ya juhudi zote zilizofanyika na hatua zilizopigwa katika miaka 20 iliyopita.

Ripoti inasema pengo la kijinsia ni kubwa hasa katika mataifa ya Kiarabu, Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara na Kusini na Magharibi mwa Asia.

Imeongeza kuwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wasichana milioni 9.5 hawatowahi kuhudhuria shule ikilinganishwa na wavulana milioni 5.

Kwa jumla watoto zaidi ya milioni 30 wa umri wa miaka 6 hadi 11 hawasiomi. Na pengo ni kubwa zaidi katika mataifa ya Kiarabu ambako asilimi 80 ya wasichana hawasomi ikilinganishwa na asilimi 16 ya wavulana .