Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nkurunzinza aahidi kuachia huru wafungwa 1,200

Nkurunzinza aahidi kuachia huru wafungwa 1,200

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa akiwa ziarani nchini Burundi amekutana kwa mazungumzo na rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, ambapo Ban amesema rais huyo ameahidi kuondoa vikwazo dhidi ya vyombo vya habari, kuwaachia huru wafungwa 1,200, na kuanzisha mazungumzo jumuishi na wadau wote wa kisiasa katika kuutanzua mgogoro wa kisiasa nchini humo. Taarifa kutoka Bujumbura, Mwandishi wetu Ramadhani KIBUGA anasimulia zaidi.

(Taarifa ya Kibuga)

Kwenye taarifa yao kwa vyombo vya habari kwanza kabisa Rais burundi Pierre Nkurunziza amekiri mchango mkubwa wa Umoja wa mataifa katika juhudi zake za kustaawisha taifa hili, na kuwa amekubaliana na mgeni wake Ban Ki Moon kuondoa changamoto njiani na kuhakikisha amani na usalama vinatawala nchini.

Sauti ya Nkurunziza:

“Wametuomba tuzidishe juhudi katika kuimarisha haki za binaadamu, kuhusu pia kupambana na ugaidi na kupiga vita umasikini pamoja na mipango mingine ambayo tunashirikiana na wafadhili ikiwa ni pamoja na mashirika ya Umoja wa mataifa . Hii itatudadia katika ujenzi wa taifa la amani na usalama”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amemchagiza Rais wa Burundi na serikali yake kuanzisha mara moja mazungumzo jumuishi na pande zote.Ujumbe huo ndio pia BAN ameuwasilisha akikutana na viongozi wa kisiasa na kujenga imani kubwa.

Sauti ya Ban

“Vurugu za kisiasa, ghasia na ukwepaji sheria, vina madhara makubwa ya kibinadamu. Viongozi wa kisiasa Burundi ni lazima wawe na ujasiri uaminifu utakaowezesha mchakato wa kisiasa, ili kuhakikisha watu wa taifa hili wanaishi tena kwa amani na kufurahia haki za bindamu.