Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushikamane tumalize madhila yakumbayo wakimbizi wa Sahrawi- Ban

Tushikamane tumalize madhila yakumbayo wakimbizi wa Sahrawi- Ban

Nimesikitishwa sana na machungu na hasira kutoka kwa wakimbizi walioko kambi ya Smara huko Tindouf nchini Algeria na cha kusikitisha zaidi ni kwamba wanaona wamesahaulika.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipozungumza Jumamosi na waandishi wa habari mjini Rabouni, Algeria baada ya kuzuru kambi hiyo iliyoko Tindouf sambamba na na kuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu wa chama cha POLISARIO Mohammed Abdelaziz.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Bwana Abdelaziz, Ban amesema amesikia kutoka kwa vijana jinsi walivyochoshwa na mazingira magumu kwenye kambi hiyo kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

''Hali ya kibinadamu ni mbaya sana. Lazima tufanye kazi pamoja kuwapatia vijana elimu nzuri, tuwapatie chakula, maji, huduma za kujisafi na kujikwamua kimaisha. Umoja wa Mataifa utashirikiana na jamii ya kimataifa. Wasahrawi wamekumbwa na tabu nyingi katika mazingira magumu. Nataka nipazie sauti dunia suala la watu hawa ambao shida zao mara nyingi zinasahaulika.''

Ban amesema amewahakikishia kuwa Umoja wa Mataifa utachukua hatua kuwakwamua kwa kuzingatia kwa ziara yake ilikuwa na malengo makuu manne.

Mosi kujionea hali halisi ili aweze kutoa mchango wake kupatia suluhu mzozo huo, pili kutembelea ofisi ya ujumbe wa umoja wa Mataifa MINURSO iliyoko Bir Lahlou na kuona shughuli zao ikiwemo kutegua mabomu ya ardhini.

Ameeleza lengo la tatu ni kuona hali halisi ya kambi ya wakimbizi wa Sahrawi karibu na Tindouf ambako amesema mazingira ni magumu sana familia zikiwa zimetanganishwa kwa muda mrefu.

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon (mwenye suti nyeusi) alipotembelea kituo cha MINURSO kinachohusika na uteguaji wa mabomu huko Bir Lahlou, Sahara Magharibi. (Picha/UN)
Lengo lake la nne ni kuhakikisha kuna usalama kwenye eneo hilo likikumbwa na uhalifu na usafirishaji wa madawa ya kulevya na hofu kuwa magaidi wanaweza kuchukua fursa ya ukosefu wa usalama kuchipuka.

Ban amesema hali ya sasa haikubali, kando mwa mchakato wa kisiasa ni lazima janga la kibinadamu lishughulikiwe na hivyo akagusia mkutano wa kiutu wa mwezi Mei huko Istanbul, Uturuki akitangaza pia azma yake ya kuitisha mkutao wa wahisani huko Geneva.

Katibu Mkuu amesema licha ya machungu wanayopata wakimbizi wa Sahrawi, ameguswa na vile ambavyo wana imani na Umoja wa Mataifa hivyo ameomba jamii ya kimataifa kuazimia kumaliza mzozano uliopo kati ya Morocco na chama cha Polisario katika kusaka suluhu la kudumu.

Mzozo ulizuka katika Morocco na chama cha Polisario mwaka 1976 baada ya Hispania kujiondoa kwenye kwenye eneo la Sahara Magharibi. Hata hivyo mwaka 1991 maridhiano yalifikiwa kati ya pande mbili hizo na ofisi ya Umoja wa Mataifa MINURSO kuanzishwa kusimamia makubaliano hayo sambamba na kura ya maoni kuhusu kujitawala kwa Sahara Magharibi.

Hata hivyo Morocco imewasilisha mpango wa kuweka jimbo hilo huru lakini POLISARIO inataka hatma ya kujitawala kwa jimbo hilo iamuliwe kupitia kura ya maoni kuhusu kujitawala na uhuru kama moja ya fursa.