Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Radio yasalia muokozi kote duniani - Ban na O B'rien

Radio yasalia muokozi kote duniani - Ban na O B'rien

Leo ni siku ya radio duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema wakati wa majanga, radio imesalia kuwa muokozi na kwamba watu walio katika majanga hukimbilia radio kusaka taarifa.

Katika ujumbe wake Ban amesema radio inasaidia wakati wa majanga na hata ujenzi wa jamii baada ya majanga.

Amegusia pia radio za kijamii akisema zimekuwa fursa ya wananchi kupaza sauti zao na hivyo amesema wakati wa huu ambapo malengo ya maendeleo endelevu yanaanza kutekelezwa, Radio itumiwe kama chombo cha kuleta maendeleo.

“Kuelekea mkutano wa usaidizi wa kibinadamu huko Istanbul mwezi Mei mwaka huu, hebu na tusake mbinu za kuwezesha radio kuweza kutoa usaidizi zaidi wakati wa majanga.”

Wakati huo huo Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa kibinadamu OCHA Stephen O’Obrien amesema kuanzia Afrika Magharibi hadi Asia, Radio imesalia muokozi hasa kwa jamii akitolea mfano Nepal.

(Sauti ya O’brien)

“Nchini Nepal ambako watu wengi hawana magazeti wala intaneti, radio ilikuwa chanzo muhimu na cha uhakaki wakati tetemeko kubwa la ardhi lilipokumba nchi hiyo mwaka jana.”

Kwa mantiki hiyo ametaka kutambuliwa kwa majukumu yanayotekelezwa na vituo vya radio zaidi ya Elfu 44 duniani kote wakati wa dharura, iwe ni vita au majanga ya asili.