Skip to main content

Mapigano mapya yawafungisha virago maelfu Darfur: UNAMID

Mapigano mapya yawafungisha virago maelfu Darfur: UNAMID

Taarifa kutoka Darfur Sudan zinasema maelfu ya wakimbizi wa ndani wanakimbilia katika miji na vijiji vya maeneo ya Kati na Kaskazini mwa Dafur kutokana na mapigano kati ya majeshi ya serikali na kundi la upinzani la Sudan’s Liberation Movement, SLM. Amina Hassan na taarifa kamili...

(TAARIFA YA AMINA)

Mpango wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID umetoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano huku ukiwa tayari kusaidia katika juhudi za kufikia suluhu ya amani ya mzozo huo.

UNAMID na mashirika mengi ya misaada ya kibinadamu ya kitaifa na kimataifa wanakimbizana na muda kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa wakimbizi hao ambao wengi ni watoto, kina mama wanaonyonyesha, wagonjwa na wazee ambapo wengi wanatembea mwendo wasaa hadi 13 kufikia kituo cha UNAMID cha Sorton.

Kaimu mkuu wa masuala ya kibinadamu wa UNAMID Zurab Alzarow anasema hali ni tete..

(SAUTI YA ZURAB)

“ Wakati huu tunapozungumza watu 14770 wamechukua hifadhi kwenye kituo cha UNAMID cha Sorton Kaskazini mwa Darfur na idadi inaendelea kuongezeka kila siku. Wengi wa watu hao kwenye kituo chetu ni watoto. Mahitaji ya dharura ni chakula, maji, madawa na mahitaji yasio chakula kama mablanketi. Timu ya UNAMID inatoa mahitaji ya msingi kwa wakimbizi hao wa ndani , walinda Amani wanagawana mlo wao na wakimbizi na kutoa huduma za afya."

Mapigano hayo yaliyoanza tarehe 16 mwezi huu bado yanaendelea na tangu mwanzo wa mwaka huu watu 250,000 wamelazimika kukimbia nyumba zao jimboni Darfur na nusu yao tu ndio waliopata msaada.