Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjini Madaya, watu wanahitaji msaada wa kuokoa maisha

Mjini Madaya, watu wanahitaji msaada wa kuokoa maisha

Timu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF iliyowasili mjini Madaya nchini Syria wiki hii imeshuhudia kifo cha mtoto wenye umri wa miaka 16 aliyeathirika na unyafuzi.

Msemaji wa UNICEF Syria Hanaa Singer amenukuliwa kwenye taarifa ya shiriki hilo akisema mtoto huyo alifariki dunia hospitalini,  huku watoto 22 wenye unyafuzi wakiwa wamebainiwa na kupewa vyakula maalum vya kuokoa maisha yao.

Aidha UNICEF imeeleza kuwa imebaini watu walio hatarini kupoteza maisha yao iwapo hawatasafirishwa kwa ajili ya matibabu.

Bi Singer ameongeza kwamba tathmini thabiti kuhusu hali ya uhaba wa chakula itaendelea kufanyika, huku akiziomba pande kinzani za mzozo kuruhusu mashirika ya kibinadamu kufikisha misaada muhimu kwa wananchi.

Amekariri kwamba licha ya kushtushwa sana na hali ya Madaya, ni muhimu kukumbuka kwamba nchini Syria kuna maeneo 14 yanayofanana na Madaya ambako watu wako hatarini kufa kwa njaa.