Skip to main content

UNICEF yahofia njaa nchini Malawi

UNICEF yahofia njaa nchini Malawi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limeanza utaratibu wa kufuatilia hali ya utapiamlo miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini Malawi, likihofia kwamba nchi hiyo inaweza kukumbwa na hali mbaya ya njaa kutokana na ukame na mzozo wa kiuchumi.

Kwa mujibu wa UNICEF, tayari watu milioni 2,8 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula nchini humo, huku ripoti zinaonyesha kwamba ukosefu wa chakula umezidi.

Mkuu wa UNICEF nchini Malawi Mahimbo Mdoe ameeleza kwamba licha ya kiasi cha kutosha cha mvua msimu huo, ukame wa miezi iliyopita umesababisha ukosefu wa chakula utakaoathiri watoto..

Aidha taarifa ya UNICEF imeeleza kwamba ukosefu wa chakula unakumba ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kusini, huku  nchi zilizoathirika zaidi zikiwa ni Ethiopia, Somalia na Zimbabwe.