Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani wa Burundi wasitisha usaidizi wa bajeti:

Wahisani wa Burundi wasitisha usaidizi wa bajeti:

Baada ya ziara nchini Burundi kujionea hali ya kibinadamu, Mkuu wa operesheni kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA, John Ging, amesema mzozo wa kisiasa umesabisha nchini humo umesababisha wahisani kusitisha msaada wa kibajeti na hivyo kuzorotesha hali ya kibinadamu na kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Bwana Ging amesema bajeti ya Burundi inategemea zaidi ya asilimia 51 kutoka kwa wahisani kwa hiyo kusitishwa kwa misaada kumeongeza shida juu ya shida.

(Sauti ya Ging)

“Wahisani wakuu wanaosaidia bajeti kama vile upatikanaji wa huduma muhimu za umma wamesitisha misaada hiyo. Kwa  hiyo basi huduma hizo sasa hivi hazina fedha, mathalani dawa muhimu, malipo ya mishahara na kadhalika.”

Bwana Ging amesema kwa sasa yaonekana hakuna mwenye jibu kwenye mzozo wa Burundi na hilo ndio tatizo kwa hiyo..

(Sauti ya Ging)

“Tunatoa wito kwa wale wenye wajibu wa kisiasa kuongeza juhudi zao maradufu! Kila mmoja anapaswa ajikite na wajibu wake, mimi najikita suala la kibinadamu lakini nina wajibu wa kupaza sauti na kusema kuwa hali ya kibinadamu inazorota, na suluhu iko wapi? Si ya kibinadamu! Sisi hatuna jibu bali ni suluhu ya kisiasa!”

Kwa mujibu wa Ging, hali ya kibinadamu inashuka kwa kasi na amenukuu ripoti ya maendeleo ya kibinamu inayoiweka Burundi nafasi ya 194 kati ya nchi 197.