UNMISS , UNIFSA zaongezewa muda hadi mwakani

UNMISS , UNIFSA zaongezewa muda hadi mwakani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu Sudan Kusini ambapo pamoja na mambo mengine limepitisha azimio la kuongeza muda wa ujumbe wake nchini humo, UNMISS hadi tarehe 31 Julai mwaka 2016.

Azimio hilo nambari S/2252/2015 pamoja na kuongeza muda limetambua majukumu ya ujumbe huo katika ulinzi wa raia na uchunguzi wa ukiukwaji wa haki za  binadamu.

Halikadhalika azimio limeongeza ukubwa wa jeshi hadi askari 13,000 na polisi 2,001 wakijumuisha maafisa wa polisi na magereza na limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuharakisha mchakato wa kupelekwa kwa watendaji hao.

Hata hivyo Urusi na Venezuela hazikuonyesha msimamo wowote juu ya azimio hilo ambapo mwakilishi wa Urusi amesema suala la vikwazo katika azimio hilo halina tija huku yule wa Venezuela akisema masuala ya mazungumzo bado hayazingatiwi vya kutosha.

Halikadhalika Baraza limekuwa na kikao kuhusu Sudan ambapo limeongeza muda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda usalama kwa muda Abyei, UNIFSA hadi Mei 15 mwakani.