Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Bilioni 20.1 zasakwa kuimarisha usaidizi duniani

Dola Bilioni 20.1 zasakwa kuimarisha usaidizi duniani

Umoja wa Mataifa na wadau wake umezindua kampeni ya kusaka dola bilioni ishirini nukta moja kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu zaidi ya milioni 87 duniani kote wanaohitaji msaada wa kibinadamu mwakani. John Kibego na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Kibego)

Licha ya kuwa na watu zaidi ya milioni 125 wanaohitaji msaada wa kibinadamu duniani kote, fedha hizo zitasaidia watu milioni 87.6 wenye uhitaji wa dharura hasa wale wanaokimbibia migogoro na wathirika wa majanga asili.

Kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo mjini Geneva Uswisi,  Stephen O’Brien msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu misaada ya kibinadamu na mratibu na mkuu wa OCHA amesema mateso duniani yamefikia kiwango cha juu zaidi katika kizazi hiki, na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kufadhili juhudi za kushugulikia mahitaji yanayozidi miongoni mwa waathirika.

(Sauti ya O’Brien)

"Kiwango cha madhila duniani ni cha juu na fedha zilizopo haziwezi kukabiliana nacho,  Tunapomaliza mwaka huu kuna pengo la ufadhili la dola bilioni 10.2. Ili kuweza kukabiliana na hali hii mbaya tunategemea wafadhili na wahisani ambao wamejitolea awali. Pamoja tutatumia fedha hizo kubadilisha maisha na kupunguza madhila ya mamilioni ya wanawake, wanaume, wasichana na wavulana."

Mahitaji yanayoangaziwa ni pamoja na yale ya msingi kama chakula, dawa, nyumba, na elimu.

Mizozo nchini Syria, Iraq, Sudan Kusini na Yemen ndio kichocheo cha uhitaji zaidi wa msaada kwa waathirika ndani na nje ya nchi hizo, huku ripoti ikisema, kwa tayari watu milioni 60 duniani kote, wamekimbia makao, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu kumalizika kwa Vita Vya Pili vya Dunia.