Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Orodha yatolewa ili kuepusha vifo vya wajawazito na watoto

Orodha yatolewa ili kuepusha vifo vya wajawazito na watoto

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema orodha mpya ya kuhakikisha usalama wakati wanawake wakijifungua inalenga zaidi sababu za vifo vya watoto na akinamama wakati wa kujifungwa katika vituo vya afya na hasa uzazi unaosimamiwa na wakunga wasio na ujuzi wa kutosha.

Shirika hilo limesema, idadi kubwa ya vifo hivyo hutokea wakati wa kujifungua na zaidi yake ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa kwa mtoto, likisisitiza kuwa vinaweza kuzuilika.

Dokta Marie-Paule Kieny, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi kuhusu mifumo ya afya na uvumbuzi ndani ya WHO amesema, vifo hivyo vinatokana na huduma mbovu za afya akionyesha matumaini kuwa orodha hiyo mpya itawasaidi wahudumu wa afya, kuzingatia utaratibu uafao kwa kila mjamzito.

Ripoti imesema, wajawazito 303,000 kati ya milioni 130 wanaojifungua kila mwaka hufariki dunia kote ulimwenguni , watoto milioni 2.6 wakifariki dunia kabla ya kuzaliwa, ilhali Milioni 2.7 wakifariki dunia katika siku 28 baada na kuzaliwa.