Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na hatua dhidi ya kauli za chuki kupitia mitandao

UM na hatua dhidi ya kauli za chuki kupitia mitandao

Umoja wa Mataifa kupitia mwakilishi wake wa ngazi ya juu kuhusu ustaarabu Nassir Abdulaziz Al-Nasser umechukua hatua kukabiliana na kuenezwa kwa kauli ya chuki kupitia mbinu mpya za mawasiliano.

Akifungua kongamano la siku moja kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York Marekani, Bwana Al-Nasser amesema vikundi vyenye misimamo mikali vinatumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kusongesha itikadi zao kali na kuchochea chuki na ghasia.

Halikadhalika ameshutumu matumizi ya teknolojia ya habari kuimarisha fikra potofu, unyanyapaa n ahata kujenga chuki baina ya watu wa rangi mbali mbali, dini na wale wanaojitambulisha kwa jinsia tofauti.

Katika mkutano huo Cristina Gallach ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya mawasiliano kwa umma, alikuwa miongoni mwa watoa mada ambapo amesisitizia hali inayoibuka hivi sasa.

"Zama za sasa kuliko wakati wowote ule, watu wanatumia ujumbe wa chuki kuchochea mvutano baina ya ustaarabu tofauti kwa misingi ya dini. Lengo lao ni kujenga misimamo mikali miongoni mwa vijana ili mtazamo wao kwa dunia uwe ni nyeusi au nyeupe, mbaya badala ya nzuri na hivyo waamua kuchagua ghasia kama njia pekee ya kupata jibu.”

Bi. Gallach amependekeza hatua mbili za kuchukua ikiwemo kutunga na kusimamia sheria za kudhibiti kauli za chuki na kutumia mbinu za mawasiliano kutuma ujumbe wa kujenga umoja kwa misingi ya ubinadamu.