Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani auawa huko CAR, Ban alaani

Mlinda amani auawa huko CAR, Ban alaani

Huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, waasi waliokuwa kikundi cha Seleka, wameshambulia askari wa kikosi cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA na kuua mlinda amani mmoja.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa makabiliano hayo yanafuatia mapigano ya awali kati ya watu hao na kikundi kinachopinga waasi wa Balaka huko Batangafo, kilometa 400 kutoka mji mkuu Bangui.

Habari zinasema askari huyo aliyeuawa, awali alipotea wakati wa tukio hilo na hatimaye maiti yake kupatikana baadaye.

Kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mauaji ya mlinda amani huyo kutoka Cameroon akisisitiza kuwa vikundi vyenye silaha visalimishe silaha zao na vijiepushe na ghasia.

Amesema MINUSCA itachukua hatua zipasazo kwa mujibu wa mamlaka yake kulinda raia na kuimarisha utulivu nchini CAR.

Ban amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora ili uchaguzi uweze kufanyika nchini humo kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na tme ya taifa ya uchaguzi na hivyo kuwezesha kumalizika kwa kipindi cha mpito na hatimaye utulivu na amani endelevu nchini humo.