Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Homa ya uti wa mgongo aina A ukingoni Afrika: WHO

Homa ya uti wa mgongo aina A ukingoni Afrika: WHO

Chanjo dhidi ya homa ya uti wa mgongo aina A iliyoanza kutumika miaka mitano iliyopita kwenye nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara imeanza kuleta matumaini kutokana na idadi ya wagonjwa na vifo kupungua. Amina Hasssan na maelezo zaidi.

 (Taarifa ya Amina)

Shirika la afya duniani, WHO limetolea mfano kuwa mwaka 2013 pekee ni visa vinne tu vya homa ya uti wa mgongo vilithibitishwa katika maabara kwenye nchi 26 zinazokumbwa na zaidi ya ugonjwa huo, zikianzia Ethiopia hadi Senegal.

WHO inasema gharama ya chanjo hiyo MenAfriVac, ni chini ya senti 50 ya dola na kila mahali ambapo imetolewa kupitia kampeni ya chanjo imeweza kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

Dkt. Marie Pierre Preziosi ni mkurugenzi wa mradi wa chanjo ya homa ya uti wa mgongo WHO anasema mafanikio yamepatakana lakini...

 (Sauti ya Dkt. Preziosi)

 “Wito wetu leo ni kusihi nchi zilizo ukanda wa homa ya uti wa mgongo kuingia mkakatiwa pili wa kujumuisha chanjo hiyo kwenye utaratibu wa utoaji chanjo, kwa kuwapatia watoto wachanga wenye umri wa kuanzia miezi Tisa hadi 18 dozi moja ya chanjo  sambamba na chanjo ya kwanza au ya  pili ya Surua.”

Chanjo hiyo ilitokana na ombi la mawaziri wa afya wa nchi za Afrika baada ya mlipuko wa ugonjwa huo mwaka 1996 uliokumba watu zaidi ya Laki Mbili na Nusu na kuua zaidi ya 2,500.