Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Haki za Binadamu lajadili haki za watu wa asili

Baraza la Haki za Binadamu lajadili haki za watu wa asili

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, limehitimisha leo mjadala wake wa siku mbili kuhusu hali za haki za binadamu zinazohitaji kumakinikiwa.

Katika mjadala wake leo, Baraza hilo limesikiliza ripoti kuhusu haki za watu wa asili, zikiwasilishwa na mtaalam maalum kuhusu haki za kundi hilo, Victoria Tauli Corpuz, miongoni mwa wengine.

Katika hotuba yake, Bi Corpuz amesema mwaka 2015 umekuwa wa kihistoria kwa watu wa asili, ingawa bado kuna changamoto kubwa katika kuziba pengo lililopo kati ya kuongezeka kwa kutambuliwa kwa haki zao katika ngazi za kitaifa na kimataifa, na kutekelezwa kwa haki hizo mashinani

Aidha, baraza hilo limesikiliza ripoti za mkakati wa wataalam kuhusu haki za watu wa asili na bodi ya mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kujitolea kwa ajili ya watu wa asili.

Akiongea kwenye mkutano huo mwakilishi wa watu wa asili Albert Kwokwo BArume kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesisitiza mchango mkubwa ulipatiwa na watu wa asili kutoka bara la Afrika licha ya changamoto zilizopo bado.

(SAUTI ALBERT)

"Hali ya watu wa asili barani Afrika bado inatia wasiwasi sana. Watu wa asili wanaendelea kulaghaiwa ardhi, ukatili dhidi ya wanawake hausitishwi, idadi ya watu wa asili wanaopata huduma za afya, elimu na ajira ni chini ya viwango vya taifa, na watoto kutoka jamii hizo hua wanakejeliwa na wengine na wanaacha shule kwa wingi.”