Shakira ashiriki na UNICEF kupigia debe maendeleo ya watoto wadogo

Shakira ashiriki na UNICEF kupigia debe maendeleo ya watoto wadogo

Elimu ya awali, upendo na lishe bora ni misingi muhimu katika kuhakikisha akili za watoto wadogo zinakuwa vizuri.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF ambalo limekuwa na tukio maalum leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, kwa ajili ya kumulika umuhimu wa maendeleo ya watoto wadogo ECD.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amezingatia umuhimu wa kuwapatia watoto wadogo huduma za elimu, lishe bora na kupambana na ukatili dhidi yao.

« Mtoto akikosa kuchangamshwa ipasavyo anapokuwa mdogo, akili zake hazitakuwa vizuri, kwa sababu kila sekunde, seli elfu moja zinaungana ubongoni mkwake. Zisipoungana, italeta tofauti kubwa sana kwenye maisha ya baadaye ya mtoto. »

Ameeleza kwamba bado watoto milioni 160 duniani kote wamedumaa, ambao hawataweza kuwa na akili na fursa sawa kama wenzao.

Kwa upande wake Balozi Mwema wa UNICEF mwanamuziki Shakira amesema kuwekeza katika maendeleo ya watoto wadogo kunaleta ufanisi mkubwa.

“ Kuwekeza katika maendeleo ya watoto wadogo kunakuza ukuaji wa uchumi, kunapunguza tofauti na kunasaidia kuondoa uhalifu na vurugu. Kwa hiyo kuna ufanisi. Bila shaka ni njia bora kuhakikisha dunia yenye utulivu, amani na maendeleo.”

Katika hotuba yake wakati wa mkutano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuwekeza katika maendeleo ya watoto wadogo hainufaishi tu watoto bali pia jamii kwa ujumla, akifuraishwa kuona kwamba swala hilo limeingizwa kwenye malengo ya maendeleo endelevu.