Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kimataifa wamulika madhara ya dawa za kulevya kwa jamii

Mkutano wa kimataifa wamulika madhara ya dawa za kulevya kwa jamii

Wawakilishi wa serikali na wataalam kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa, pamoja na mashirika ya kikanda na asasi za kiraia, wanakutana mjini Mexico kubadilishana mawazo kuhusu uzoefu wao katika kukabiliana na madhara ya masoko haramu ya dawa kijamii, kama vile ukatili, misongamano ya watu jela, utelekezaji na kudhoofika kwa mifumo ya kijamii.

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika kabla ya kikao maalum cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu tatizo la dawa duniani mnamo mwezi Aprili mwakani.

Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu dawa na uhalifu, UNODC, unajadili mienendo, hatua zinazochukuliwa, pamoja na mafunzo yanayotokana na jinsi ya kuzuia na kupatia mwarobaini madhara ya kijamii yatokanayo na masoko haramu ya dawa, katika mkakati wa mikataba na vyombo vya Umoja wa Mataifa.