Skip to main content

Hofu ya kirusi Zika, WHO yaitisha mkutano.

Hofu ya kirusi Zika, WHO yaitisha mkutano.

Shirika la Afya Duniani, WHO tarehe 28 mwezi huu litaitisha mkutano maalum kuhusu kirusi aina ya Zika. Amesema leo msemaji wa WHO Christian Lindmeier, wakati huu ambapo kirusi hicho tayari kimeripotiwa kwenye nchi 20 huku Brazil ikiwa ni nchi iliyoathirika zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Bwana Lindmeier ameeleza kwamba kirusi chenyewe cha Zika si hatari, kwani huhasababisha tu ukurutu mwilini.

Hata hivyo ameeleza kwamba Brazil imeshuhudia pia visa 4,000 vya watoto wanaozaliwa na vichwa vidogo, miongoni mwao 49 wakiwa wamefariki dunia, ikidaiwa hali hiyo kuwa na uhusiano na kirusi cha Zika.

Bwanza Lindmeier ameongeza kwamba WHO sasa inaendesha utafiti kuthibitisha iwapo kuna uhusiano kati ya Zika na tatizo hilo ambapo akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa amesema..

(sauti ya Bwana Lindmeier)

“ Iwapo uhusiano utathibitishwa, itakuwa hali ya kutia wasiwasi sana, kwa sababu inaathiri wakinamama na watoto nchini Brazil. Lakini hadi sasa tumeshuhudia vichwa vidogo nchini Brazil tu, hatujashuhudia vichwa vidogo kwenye nchi zingine.”

Aidha amesema kwamba WHO haijapendekeza wanawake kujikinga dhidi ya kupata mimba, akieleza kwamba suluhu dhidi ya kirusi cha Zika hivi sasa ni kujikinga na mbu aina ya Aedes, ikiwa ni Brazil au kwingineko.