Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ireland kupiga jeki shughuli za WFP Uganda

Ireland kupiga jeki shughuli za WFP Uganda

Serikali ya Ireland imeahidi kupiga jeki ya dola $800,000 kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya kusaidia watoto wa shule katika eneo linalokabiliwa na njaa kali la Karomoja Kaskazini Mashariki mwa Uganda na wakimbizi walioko nchini humo. John Kibego na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Kibego)

Katika mkataba wa makubaliano uliyotiiwa saini na Mkurugenzi wa WFP Michael Dunford na Balozi wa Ireland nchini Uganda Donal Cronin, mchango huo utasaidia kulisha watoto 100,000 na wakimbizi 150,000 wa Sudan Kusini walioko Kaskazini mwa nchi.

Mkurugenzi Danford amesema, WFP itatumia fedha hizo kununua chakula kama mahindi na maharagwe kutoka kwa wakulima wadogo nchini humo.

Ameonyesha matumaini kuwa, uwepo wa milo ya watoto shuleni ketika eneo lenye njaa la Karamoja utasaidia kuongeza idadi ya wanaoingia shuleni na kubaki wakisoma.

Serikali ya Ireland imetoa ahadi hiyo wakati ambapo WFP inakabiliwa na changamoto ya ufadhili kutokana na kumiminika kwa wanaokimbia mapigano hasa nchini Sudan Kusini.

Mwisho.