Skip to main content

Tubadilike tunavyoshughulikia ukiukwaji haki la sivyo hatuna umuhimu: Zeid

Tubadilike tunavyoshughulikia ukiukwaji haki la sivyo hatuna umuhimu: Zeid

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeanza kikao chake cha 30 mjini Geneva Uswisi ambapo Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja huo Zeid Ra’ad Al Hussein amesema mwaka mmoja tangu ashike wadhifa huo, kiwango cha machungu duniani kinazidi kuongezeka kila uchao na uwezo wa dunia kushughulikia inatia hasira. Taarifa zaidi na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Kamishna Zeid amesema hakuna cha kudhihirisha hali hiyo zaidi ya picha ya mtoto wa Aylan Al Kurdi kutoka Syria ambaye mwili wake ulikutwa ukielea kwenye pwani ya Uturuki baada ya safari ndefu ya kukimbia machungu nchini mwake.

Amesema kama hiyo haitoshi, ubaguzi umezidi kushamiri, umaskini, ukiukwaji wa haki za binadamu na hata mateso huku jamii ya kimataifa ikishindwa kuchukua hatua, hivyo akasema...

(Sauti ya Zeid)

“Labda tubadilishe kabisa mtazamo na fikra zetu kama jamii ya kimataifa, nchi wanachama, mashirika ya kiraia na yale ya kimataifa katika jamii hii ya haki za binadamu. La sivyo sote tutasalia hatuna umuhimu wowote katika zama hizi za ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu.”