Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

We Care Solar yashinda tuzo ya dola milioni moja kwa ajili ya kukuza nishati endelevu

We Care Solar yashinda tuzo ya dola milioni moja kwa ajili ya kukuza nishati endelevu

Kwenye maadhimisho yaliyofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York Marekani, Shirika lisilo la kiserikali la We Care Solar lenye makao makuu huko Carlifornia, limeshinda tuzo ya dola milioni moja kutokana na mradi wao wa kuimarisha afya ya watoto na wakina mama kupitia huduma za umeme utokakanao na nishati ya jua.

Tuzo hiyo inayoitwa “Powering the future we want, yaani “ kukuza mustakhabali tunaotaka”, iliyoanzishwa mwaka huu na Umoja wa Mataifa, inalenga kumulika jitihada zinazofanyika katika kukuza nyenzo endelevu ya upatikanaji wa nishati.

Akiongea kwenye maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema upatikanaji wa nishati ni msingi katika juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

“ Najua adha ya kukosa nishati ya kisasa. Nilipokuwa mtoto, nilikuwa nasoma kwa kutumia mshumaa au taa ya mafuta. Leo bado mtu mmoja kati ya watano anakosa umeme. Tunahitaji kuwezesha kila mtu kupata huduma za nishati ya kisasa.”

Katibu Mkuu akasisitiza kwamba upatikanaji wa nishati unapaswa kuimarishwa kwa njia endelevu, ili kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, na kwa hivo kubadilisha njia ya kutumia nishati, ikiwa ni lengo nambari saba la malengo ya maendeleo endelevu yatakayopitishwa mwisho wa mwezi huu.