Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa taarifa kuhusu mustakhabali wa operesheni za ulinzi wa amani

Ban atoa taarifa kuhusu mustakhabali wa operesheni za ulinzi wa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa leo ajenda yake kuhusu mambo ya kipaumbele katika operesheni za ulinzi wa amani na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuyatimiza.

Hii ni kufuatia kutolewa kwa ripoti kuhusu mustakhbali wa operesheni za ulinzi wa amani, kufuatia kazi ya jopo la ngazi ya juu lililoteuliwa mnamo Oktoba 2014, likiongozwa na Rais wa zamani wa Timor-Leste, Jose Ramos-Horta, ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Guinea Bissau.

Ban amesema operesheni za ulinzi wa amani zinapaswa kubadilishwa ili zilingane na changamoto za sasa na za siku zijazo, akitaja mambo matatu muhimu. Mosi, amesema kuna haja ya kutoa kipaumbele kwa kuzuia na upatanishi ili kuvunja mzunguko wa kuchukua hatua za kuchelewa na zenye gharama kubwa. Pili, amesema kuna haja ya kubadili jinsi ya kupanga na kufanya operesheni za ulinzi wa amani, ili kuzifanya ziwe na kasi na kuwajibika kwa nchi na watu. Na tatu, kuunda mkakati wa kimataifa na kikanda ili kushughulikia changamoto za leo za amani usalama.