Skip to main content

Misukosuko Guinea-Bissau yasababisha UNIOGBIS kuchukua hatua mpya

Misukosuko Guinea-Bissau yasababisha UNIOGBIS kuchukua hatua mpya

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini Guinea Bissau Miguel Thunderstorm, Ijumaa amelihutubia Baraza la Usalama jijini New York akisema mwaka mmoja tangu kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba nchini humo, nchi hiyo imejikuta ikitumbukia katika misukosuko ya kisiasa.

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali nchini Guinea Bissau na shughuli za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNIOGBIS ambao pia yeye ndiye anaongoza, mwakilishi huyo amesema misukosuko hiyo inadhihirishwa na hali halisi ikiwemo Rais kumuondoa madarakani Waziri Mkuu mwezi Agosti mwaka huu na kumteua waziri mwingine kushika wadhifa huo.

Amesema kinachoendelea sasa ni marejeo ya ripoti za awali kuwa bado mzizi wa mzozo Guinea Bissau haujashughulikiwa vya kutosha ili kuweza kumaliza ukosefu wa imani baina ya vyama kinzani na hatimaye maendeleo thabiti yaweze kupatikana.

Bwana Thurnderstom amesema kwa kuzingatia hali ya sasa amechukua hatua ikiwemo..

(Sauti ya Thunderstorm)

“Mara kwa mara nimekuwa nawasiliana na wawakilishi waandamizi wa umma, raia na vyama vya siasa na kwa kuzingatia maendeleo ya hivi karibuni, nimeimarisha vikao vyangu na hivi vyama kwa lengo la kuhamasisha pande husika kupatia kipaumbele mashauriano kama njia bora zaidi ya kumaliza tofauti baina yao.”

Mkuu huyo wa UNIOGBIS amesema jamii ya kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa imesalia kidete kusaidia nchi hiyo inapoelekea kujiletea maendeleo akisifu jitihada zinazoongozwa na Katibu Mkuu Ban Ki-moon na jumuiya ya uchumi ya  nchi za Afrika Magharibi.