Watoto wengine 163 waachiliwa huru huko CAR leo:UNICEF

Watoto wengine 163 waachiliwa huru huko CAR leo:UNICEF

Huko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, watoto wengine 163 wakiwemo wasichana Watano wameachiliwa huru leo Ijumaa na kundi lililojihami la Anti-Balaka.Taarifa kamili na Joseph Msami.

(Taarifa ya Msami)

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo Mohamed Malick Fall amesema watoto hao wamekabidhiwa katika mji wa Batangafo na kufanya idadi ya watoto walioachiliwa huru na vikundi vilivyojihami tangu mwezi Mei mwaka huu kufikia zaidi ya 600.

Amesema tukio la leo ni kiashiria kuwa mchakato wa kutekeleza ahadi zilizotolewa na viongozi wa vikundi hivyo kama sehemu ya mpango wa amani wa mwezi Mei, unafanya kazi ipasavyo.

Watoto hao baada ya kuachiliwa huru walipatiwa huduma za matibabu na kuzungumza na wahudumu wa ustawi wa jamii na tayari wamepelekwa kwenye kituo cha mpito ili waweze kujiunga na shule au vyuo vya ufundi, huku taratibu za kuwaunganisha na familia zao zikiendelea.

Makabidhiano ya leo yaliwezekana kufuatia ushirikiano kati ya UNICEF na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, MINUSCA.