Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbegu za asili za viazi zahifadhiwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo

Mbegu za asili za viazi zahifadhiwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo

Harakati za kuhifadhi mbegu za asili za mazao kwa vizazi vijayo zimeendelea leo ambapo aina 750 ya mbegu za viazi zilizodhaniwa kutowekea huko Amerika Kusini zimejumuishwa katika hifadhi kuu ya dunia ya mbegu kaskazini zaidi mwa ncha ya kaskazini mwa dunia.

Hifadhi hiyo ya Svalbard iko chini ya barafu na tayari ina mbegu zaidi ya Laki Nane na Elfu Sitini za mazao ya chakula kutoka nchi mbali mbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva, akiungana na wanasayansi na wawakilishi kutoka Peru, Costa Rica na Norway wameshuhudia tukio hilo lililofanywa na watu wa jami ya asili ya Andea kutoka Peru.

Ukusanyaji wa mbegu hizo 750 za asili za viazi umetokana na mradi wa manufaa ya pamoja uliofadhiliwa na FAO huku wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Costa Rica wakijumuisha mbegu za viazi pori.

Mradi wa Svalbard unaendeshwa kwa ufadhili kutoka fuko la dunia la mbegu na serikali ya Norway.