Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasaka hifadhi Ulaya waepushwe na wasafirishaji haramu: Guterres

Wasaka hifadhi Ulaya waepushwe na wasafirishaji haramu: Guterres

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR António Guterres amesisitiza tena umuhimu wa kuwalinda dhidi ya wasafirishaji haramu wa binadamu, wakimbizi wanaokwenda Ulaya kusaka hifadhi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Bwana Guterres amesema kwa mantiki hiyo ni vyema kukawepo na mfumo thabiti wa kuwawezesha wanasaka hifadhi kihalali, akitolea mfano wakimbizi wa Syria.

Amesema mfumo huo utachukua nafasi ya mkakati wa sasa wa Muungano wa Ulaya wa kushughulikia wimbi la wakimbizi Ulaya, mkakati ambao amesema haufanyi kazi ipasavyo na kuhatarisha maisha ya wakimbizi.

(Sauti ya Guterres)

“Na katika muktadha huo nadhani ni lazima tuharakishe utekelezaji wa uamuzi uliopitishwa na baraza la Muungano wa Ulaya kuhusu ajenda ya uhamiaji. Maswali ya msingi kama vile kuwapokea, kuwasajili, maeneo muhimu kama vile kutofautisha kati ya wale wanaohitaji hifadhi na wasiohitaji na hatimaye kusaidia kurejesha makwao wale wasiohitaji hifadhi.”

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve.