Skip to main content

UNDP yazindua shindano kuhusu mabadiliko ya tabianchi

UNDP yazindua shindano kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, limezindua leo shindano la uandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ambalo litatoa fursa kwa washindi wawili kufadhiliwa kwenda kushiriki na kuandika kuhusu kongamano la kimataifa kuhusu tabianchi, COP21 mjini Paris, mwezi Disemba.

Taarifa ya UNDP inayotangaza shindano hilo imesema, huku mabadiliko ya tabianchi likiwa ni suala la dunia nzima, linayaathiri zaidi maeneo maskini zaidi duniani, na jamii za pembezoni hata zaidi. Mabadiliko ya tabianchi tayari yanaathiri afya ya mwanadamu, shughuli za biashara, na kutishia haki za binadamu za msingi kama vile kupata maji safi na uhakika wa kuwa na chakula.

UNDP imesema, ingawa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri jamii mashinani katika nchi za kipato cha chini na cha wastani, hadithi kuhusu madhara yake na suluhu ambazo serikali, jamii na watu binafsi wanatekeleza huwa zinaghubikwa na mjadala wa dunia kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Shindano la hadithi la UNDP linalenga kuchangia uongezaji uelewa wa umma kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi dhidi ya watu na jamii, pamoja na fursa na suluhu zinazoonekana katika vitendo vya watu na serikali katika nchi zinazoendelea zilizo hatarini.

Shindano linawalenga vijana wenye umri chini ya miaka 35 kutoka nchi zinazoendelea, ambao tayari wanafanya kazi na vyombo vya habari na ambao huandika kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa maelezo zaidi, tembelea tovuti: http://www.europe.undp.org/content/geneva/en/home/partnerships_initiati…