Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa IAEA akutana na Baraza la Seneti Marekani kuhusu nyuklia Iran

Mkuu wa IAEA akutana na Baraza la Seneti Marekani kuhusu nyuklia Iran

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, Yukiya Amano, amekutana leo na Kamati ya Seneti ya Marekani kuhusu masuala ya nje na kujadiliana nao kuhusu umuhimu wa jukumu la IAEA la kufuatilia na kuhakiki masuala yanayohusiana na nyuklia, chini ya Mpango wa Kina wa Pamoja wa kuchukua hatua.

Akikutana na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Bwana Amano amesema wamejadili pia kuhusu mkakati uliokubaliwa kati ya IAEA na Iran wa kutatua masuala yaliyokuwa ya utata zamani.

Amesema alilielezea Baraza la Seneti kuhusu jinsi mikataba miwili itakavyoimarisha kazi ya IAEA ya kuhakiki hatua za Iran.

Kwa upande mmoja, amesema mpango wa kina wa pamoja wa kuchukua hatua utawezesha IAEA kutekeleza makubaliano ya ziada na Iran, na hivyo kuliwezesha shirika hilo kufikia vituo zaidi na kupata taarifa zaidi. Utaitaka pia Iran ichukue hatua zingine za wazi, na hivyo kuwezesha kujua zaidi kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Nayo makubaliano ya kimkakati yatawezesha kubainisha masuala ambayo hayakukamilishwa kuhusu uwezekano wa kutumia mpango wa Iran wa nyuklia kwa sababu za kijeshi.