Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shirika la APHRC Kenya lapewa tuzo ya idadi ya watu

Shirika la APHRC Kenya lapewa tuzo ya idadi ya watu

Kituo cha Utafiti kuhusu Afya na idadi ya watu barani Afrika, APHRC kimepewa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu ya Mwaka 2015 katika hafla maalum iliyofanyika kwenye Umoja wa Mataifa.

APHRC ni Shirika lenye makao makuu mjini Nairobi Kenya, lililoanzishwa mwaka 1995 kwa ajili ya kusaidia uundwaji sheria kupitia utafiti, na tayari linafuatilia karibu miradi 40 na kuwasaidia mamia ya watafiti kutoka barani Afrika kutimiza uzamivu wao au Phd na kuchangia katika maswala ya maendeleo.

Katika mahojiano na idhaa hii, Alex Ezeh, mkurugenzi mtendaji wa APHCR, amesema tafiti zao zimesaidia nchi mbalimbali kubadili sera zao akitolea mfano Kenya..

“ Tunaweza kuangalia kazi tuliyofanya nchini Kenya kuhusu utoaji mimba usio salama. ambayo inabadili sera. Tumetoa ripoti hi mwaka 2013 ikionyesha visa karibu 500,000 vya utoaji mimba usio salama vinatokea nchini humo. Hiyo imesaidia sana kwenye utungaji wa sera na miongozo ya maendeleo kuhusu jinsi ya kukabiliana na changamoto hiyo na hali hiyo.”

Tuzo hiyo inatolewa kila mwaka kwa watu au mashirika yanayo changia kwa kiasi kikubwa katika maswala ya idadi ya watu na afya ya uzazi.