Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yasisitiza Al Bashir akamatwe afungwe

ICC yasisitiza Al Bashir akamatwe afungwe

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC Fatou Bensouda amesema kwamba raia wa Darfur nchini Sudan wanaendelea kuteseka wakati Rais wa nchi hiyo Omar Al Bashir anaendelea kukwepa amri ya ICC ya kumkamata.

Akihutubia Baraza la Usalama leo, Bi Bensouda ameanza kwa kueleza sababu zilizofanya mahakama yake itake kukamatwa kwa rais huyo wa Sudan, akisema mojawapo ilikuwa ni ripoti ya Muungano wa Afrika ya mwaka 2009 iliyomulika uhalifu wa kibinadamu uliotekelezwa Darfur, ikiwemo ubakaji, mateso na kulazimisha raia kuhama kwa nguvu.

Mwendesha mashtaka huyo ameendelea kusema kwamba raia wa Darfour wanastahili kupewa haki, akisema :

“ Raia wasio na kosa wanaendelea kuathirika na ukosefu wa usalama na utulivu, hasa kwa sababu ya kinachoonekana kuwa kampeni ya serikali inayowalenga. Wale watu wanaodaiwa kuwajibika katika uhalifu huo ni wale wale ambao wanatakiwa kukamatwa. Ni wazi kwamba wakikamatwa na kupelekwa mbele ya sheria ni njia ya pekee ya kusitisha uhalifu huo. »

Akigusia kitendo cha hivi karibuni cha Rais Al Bashir kuondoka haraka Afrika Kusini ili kukwepa kukamatwa, Bensouda amesema ni dalili ya kuonyesha uwepo wa ICC ya kutaka kumkamata rais huyo, akiziomba nchi wanachama kutekeleza amri hiyo na kumpeleka Bashir mbele ya sheria ili ahukumiwe.

Halikadhalika amesikitishwa na kuona kwamba Baraza la Usalama limeshindwa kuchukua hatua dhidi ya Sudan ili iheshimu amri ya ICC, akisema ukosefu wa utashi wa Baraza hilo unaweza kuzidi kudhoofisha uamuzi wake