Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lalaani shambulio mjini Mogadishu

Baraza la usalama lalaani shambulio mjini Mogadishu

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulio la Jumatano kwenye mji mkuu wa Somalia Mogadishu, ambalo limesababisha vifo na majeruhi.

Katika taarifa yake Baraza pamoja na kulaani limetuma salamu za rambirambi kwa wahanga wa shambulio hilo dhidi ya msafara wa usaidizi wa kibinadamu ukiwa na wanadiplomasia kutoka Falme za kiarabu.

Wajumbe wamesema shambulio hilo lililosababisha vifo vya raia wasio na hatia linakwamisha majukumu ya watendaji  hao, sanjari na harakati za Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo wamesema tukio hilo ambalo kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab kimedai kuhusika nalo, halitakwamisha harakati za baraza hilo la kutokomeza ugaidi kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wamerejea azma yao ya kuendelea kusaidia harakati za amani na utulivu Somalia zinazochagizwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini  humo UNSOM na ule wa Muungano wa Afrika, AMISOM.