Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvamizi kaskazini mwa Mali umekiuka haki za kijamii, kitamaduni na kiuchumi: Ripoti

Uvamizi kaskazini mwa Mali umekiuka haki za kijamii, kitamaduni na kiuchumi: Ripoti

Naibu Kamishna Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Kyung-wha Kang ametoa ripoti yake kuhusu hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Mali na kueleza kuwa hali ni ya kutisha ambapo waasi wa kikundi cha MNLA walifanya mauaji ya raia kwa minajili ya tafsiri ya sheria ya kiislamu, Sharia.  Ripoti hiyo ya uchunguzi uliofanyika kati ya mwezi Januari hadi Novemba mwaka jana ameiwasilisha katika kikao kinachoendelea cha Baraza la Haki za binadamu huko Geneva ambapo amesema inaonyesha ukiukwaji wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.  Kyung amesema kitendo cha jeshi kuingilia kati hivi karibuni kilifuatiwa na ghasia kubwa zilizosababishwa na askari wa jeshi la serikali ambao walionekana kuwalenga watu wa jamii ya Peuhl, Tuareg na wenye asili ya kiarabu kwa madai kuwa wanaunga mkono vikundi vya waasi wenye silaha.

(SAUTI YA Kyung)

“Tuhuma za kuhusika kwa baadhi y a askari wa jeshi la Mali kwenye vitendo vya kulipiza kisasi dhidi ya raia ni lazima zichunguzwe na wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Mipango inaandaliwa ili kuimarisha uwezo wa kudhibiti haki za binadamu nchini Mali. Hadi mwezi uliopita, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilipeleka ujumbe wake wa awali kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Mali, UNOM. Taratibu zinaendelea ili kuimarisha kikundi hicho haraka kwa lengo la kuondoa pengo kabla ya uamuzi wa hatma ya uwepo wa Umoja wa mataifa nchini Mali.”

Naye Waziri wa sheria wa Mali Malick Coulibaly amesema ripoti hiyo imeonyesha dhahiri shahiri ukiukwaji wa haki za binadadamu nchini humo na jinsi hali ilivyokuwa mbaya.