Skip to main content

Walinda amani wa MINUSCA wadaiwa kufanyia watoto ukatili wa kingono

Walinda amani wa MINUSCA wadaiwa kufanyia watoto ukatili wa kingono

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika Kati, CAR, MINUSCA umesema umepokea ripoti za tuhuma za ukatili wa kingono unaodaiwa kufanywa na moja ya kikosi chake cha walinda amani dhidi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye mji mkuu Bangui.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa tayari nchi ambamo kwayo askari hao wanatoka imejulishwa na uchunguzi wa tukio hilo umeanza na kwamba..

(Sauti ya Dujarric)

 Huduma za kitabibu na usaidizi zimeanza kutolewa kwa waathirika wa ukatili huo wa kingono na iwapo tuhuma hizo zitathibitishwa, kitendo hicho kitakuwa ukiukwaji mkubwa wa misingi ya Umoja wa Mataifa na kanuni za utendaji za walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Nchi husika itatakiwa kuchukua hatua haraka za kinidhamu.”

Tukio hilo linakuja wakati huu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunda jopo huru la kupitia vile ambavyo umoja huo ulishughulikia madai ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto CAR yaliyodaiwa kufanywa na askari wa Ufaransa ambao  hawakuwepo chini ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa.