Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utapiamlo wateketeza dola Milioni 800 kila mwaka Burkina Faso: Utafiti

Utapiamlo wateketeza dola Milioni 800 kila mwaka Burkina Faso: Utafiti

Utapiamlo miongoni mwa watoto nchini Burkina Faso unagharimu zaidi ya dola Milioni 800 kila mwaka, hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya utafiti ulioendeshwa na Muungano wa Afrika, Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP na wadau wengineo.

Gharama hizo hutokana na vifo vya watoto, huduma za nyongeza za afya kwa watoto wenye utapiamlo sanjari na kushindwa kwao kuhudhuria masomo, halikadhalika wazazi na walezi wao kushindwa kushiriki shughuli za uzalishaji ili waweze kuhudumia watoto wao.

Msemaji wa WFP Elisabeth Byrs akizungumza na waandishi wa habari Geneva, Uswisi kuhusu utafiti huo amesema utapiamlo unaenda mbali zaidi na kusababisha mtoto kudumaa pindi anapokosa viinilishe muhimu kama vile vitamin, madini na protini kwa hiyo..

(Sauti ya Byrs)

“Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa utapiamlo siyo tu suala la kijamii bali pia kiuchumi. Kwa hiyo matokeo yameonyesha umuhimu wa kupatia kipaumbele suala la utapiamlo kwenye mpango wa kitaifa kwa maendeleo.”

Kwa mujibu wa utafiti huo uitwao gharama ya njaa Afrika, athari za utapiamlo wa watoto nchini Burkina Faso, idadi ya watoto waliodumaa nchini Burkina Faso imeongezeka zaidi wakati huu ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita.