Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama Mali bado ni tete, licha ya hatua za kisiasa

Hali ya usalama Mali bado ni tete, licha ya hatua za kisiasa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na kikao kuhusu hali nchini Mali, ambapo imeelezwa kuwa licha ya hatua zilizopigwa kufikia sasa kisiasa, hali ya usalama nchini humo bado ni tete.

Akilihutubia Baraza hilo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, Mongi Hamdi, amesema kuwa ukiukaji wa hivi karibuni wa makubaliano ya kusitisha mapigano na machafuko ni ukumbusho bayana wa hali kanganyifu na isotabirika ya mazingira ya usalama katika maeneo ya kaskazini mwa Mali.

“Wimbi la hivi karibuni la machafuko katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Mali limesababisha watu wengi kuhama makwao. Ongezeko hili la wakimbizi linaweka mzigo mkubwa hata zaidi kwa rasilmali za familia za wenyeji, huduma za afya na elimu, pamoja na miundo mbinu ya maji na kujisafi.”

Ameongeza kuwa makubaliano ya amani yaliyosainiwa karibuni yamefungua matumaini ya Mali kujikwamua na matarajio ya muda mrefu ya kuondoa matatizo yaliyosababishwa na mzozo wa kisiasa na kiusalama.

“Nakaribisha kujiondoa kwa kundi la Plateforme kutoka Menaka, ambako MINUSMAH inaendelea kuimarisha uwepo wake, na kusaidia mikakati ya kuhakikisha ulinzi wa raia. Vipengele vya makubaliano ya amani vikitekelezwa kwa wakati, kwa njia jumuishi na ya maafikiano na pande husika, vinaweza kuchangia vyema juhudi zetu za kuimarisha maeneo ya kaskazini.”

Amesema Umoja wa Mataifa utachangia kwa kiwango kikubwa katika juhudi hizo, na kwamba ufanisi wa juhudi hizo za pamoja utategemea ari na utashi wa pande husika kulegeza misimamo kwa ajili ya maslahi ya raia wote wa Mali.