Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabaki ya wahamiaji 18 yabainika kwenye jangwa la Sahara

Mabaki ya wahamiaji 18 yabainika kwenye jangwa la Sahara

Serikali ya Niger kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM wamebaini mabaki ya miili ya wahamiaji 18 kwenye jangwa la Sahara.

IOM inasema yawezekana wahamiaji hao wakiwemo wanaume 17 na mwanamke mmoja, walifariki dunia wiki moja iliyopita kutokana na upepo na joto kali jangwani na hivyo kukosa maji mwilini baada ya kupotea wakati wakisafiri kuelekea Algeria.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Lacy Swing amesema kubaini kwa miili hiyo ni ishara ya hatari nyingi zisizofahamika ambazo wahamiaji wanapitia kabla ya kuweka rehani maisha yao bahari ya Mediteranea ili kufika Ulaya.

Amesema jangwa la Sahara linaweza kuwa hatari kama ilivyo bahari hiyo na kwamba visa vingin haviripotiwi.

Kwa mujibu wa IOM wahamiaji hao walitoka Niger, Mali, Côte d'Ivoire, Senegal, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Guinea na Algeria.