Viongozi wa kidini wanaweza kuchangia amani na maridhiano- Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa viongozi wa kidini, ziwe zile za kijadi au zisizo za kijadi, wana jukumu kubwa wakati huu ambapo mamilioni ya watu wanakabiliwa na matishio ya migogoro, ugaidi, uhalifu wa kupanga, ulanguzi wa dawa za kulevya na majanga ya afya. Taarifa kamili na Joshua Mmali
Taarifa ya Joshua
Ban amesema hayo akilihutubia kongamano la viongozi wa dini za dunia na zile za kijadi mjini Astana, Kazakhstan, ambalo linachagiza mazungumzo kwa ajili ya amani na maendeleo wakati huu wa misukosuko.
Ban amesema, wakati wa misukosuko, viongozi wa kidini wanaweza kutoa mwongozo unaotokana na maadili, kuleta watu pamoja na kuweka mazingira ya kujenga amani, kwa kupigia debe mazungumzo na kwa kutumia mamlaka yao ya kiroho kuwashawishi watu kutenda vitendo vya kiutu.
Katibu Mkuu amesema viongozi wa kidini duniani, ni lazima wawafundishe wafuasi wao maana kamili ya maridhiano, uelewa na kuheshimiana. Ameongeza kuwa viongozi hao wana wajibu wa kupaza sauti pale wanaojidahi kuwa wafuasi wa imani zao wanapotekeleza uhalifu kwa jina la dini.