Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udhibiti wa mauaji ya kimbari bado safari ni ndefu: Dieng

Udhibiti wa mauaji ya kimbari bado safari ni ndefu: Dieng

Jumuiya ya kimataifa iongeze juhudi kuhakikisha mauaji ya kimbari kama yale yaliyotokea Rwanda na Bosnia-Herzegovina hayajirudii tena, na hiyo ni kauli ya Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya mauaji ya kimbari, Adama Dieng.

Bwana Dieng ametoa ushauri huo wakati wa mjadala wa wazi kwenye siku ya kwanza ya kikao cha 22 cha Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

(SAUTI YA ADAMA)

"Je twaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa tumeweza kuzuia mauaji ya kimbari yasitokee tena? Jibu ni hapana! Changamoto bado ni nyingi mbele yetu. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, kwenye maeneo mengi tumeshuhudia maisha ya watu yakipotea pindi uhalifu wa kupindukia unapotokea. Nazunumzia kupotezwa kwa maisha ya maelfu ya watu huko Cambodia, Sierra Leone, Sri Lanka, Congo na Kenya. Hii ni mifano michache tu ya nchi ambako ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umefanyika na unyanyasaji umefanyika.”

Halikadhalika amegusia Mali na Syria ambako amesema ana wasiwasi mkubwa na kuonya kuwa kuna uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi.